Roho
Roho ni umbile la pekee lisiloonekana ambalo linasadikiwa kuwemo pamoja na mwili katika binadamu na kuunda hasa malaika (ambao kati yao wale wabaya wanaitwa mashetani).
Katika lugha mbalimbali umbile hilo linafananishwa na upepo au pumzi.
Katika Ukristo
[hariri | hariri chanzo]Mungu mwenyewe anasadikiwa kuwa roho bora. Kwa namna ya pekee Ukristo unasadiki moja ya nafsi za Kimungu ndani ya Utatu inayoitwa Roho Mtakatifu.
Pengine roho inafikiriwa kueleza tofauti kubwa mno ambayo inajitokeza kati ya binadamu na sokwe na wanyama wengine wote upande wa akili na utendaji, na ambayo haielezwi vya kutosha na tofauti katika DNA zao.
Inasadikiwa kuwa roho ndiyo sehemu bora zaidi ya mwanadamu na husadikiwa kuwa haifi bali hudumu milele. Roho humuunganisha mtu na ulimwengu wa kiroho ambao aghalabu huwa ni ulimwengu usioonekana na macho ya kawaida, yaani ya mwili.
Katika Uislamu
[hariri | hariri chanzo]Roho ni katika viumbe ambavyo vimeumbwa na Allāh mtukufu, na hakuna mwenye ujuzi wa kujua namna wala umbile la kitu hiki isipokuwa yeye Muumbaji. Na hata walipojaribu watu kumuuliza Nabii kuhusu jambo hili aliambiwa awajibu kuwa hii ni amri ya Mola wangu wala hawakupewa elimu ya hiyo roho isipokuwa ni chache tu. Hili ni umbile lisiloonekana ambalo kwa hakika linajulikana kuwemo pamoja na mwili katika miili ya viumbe hai wakiwemo wanadamu, majini, malaika, wanyama na mimea.
Na hii roho hutolewa kutoka kwa kiumbe husika na hapo ndiyo inaaminika kuwa ameshakufa, kwa maana hana roho. Na hii roho ni katika amri za Allah ambazo anaamrisha "kuwa na zikawa", na hizi roho zinapulizwa kwa viumbe pindi wanapokuwa kwenye matumbo ya mama zao na hapo ndipo inaaminika kuwa wanapata uhai, na pale zinapoondolewa ndipo inaaminika kuwa wanakufa.
Na alisema Allah mtukufu "hakuna nafsi inayokufa isipokuwa kwa ruhusa (idhini) yake kwa muda uliowekwa". Na yeye ana uhai usiokatika, ni wa milele.
Roho za binadamu zimeumbwa kwa ajili ya kubakia milele na milele isipokuwa kuna vipindi miili yao itapitia kama vile kuzaliwa, kukua, kuzeeka, kufa na kuoza, na baada ya hapo kurejeshewa roho zao na kufufuliwa kwa ajili ya malipo ya siku ya Malipo na baada ya hapo kuna kubakia milele aidha ni katika bustani za starehe au katika mashimo ya adhabu ya moto.
Roho haihusiani kabisa katika kutofautisha baina ya mwanadamu na wanyama isipokuwa kinachotofautisha ni akili ambayo ndio mhimili wa kumbukumbu na mazingatio na utendaji. Na katika kutofautisha baina ya wanyama na wanadamu ilitofautishwa kwa kutumia ufahamu na kuzingatiaji kama alivosema Mola Muumba wa vyote "wana nyoyo na hawatumii nyoyo hizo ili kufahamu na wana masikio na hawatumii masikio kusilizia, basi hao ni kama wanyama au watakuwa ni zaidi ya wanyama kwa kupotea".
Inaaminika kuwa roho ndiyo sehemu bora zaidi ya mwanadamu na sio roho tu bali ni moyo na husadikiwa kuwa roho haifi bali hudumu milele. Roho sio kitu kinachomuunganisha mtu na ulimwengu wa ghaibu bali ni imani ndiyo inayomfanya mtu aamini mambo ya ghaibu (siri) yasiyoonekana kama vile kuamini kuwa malaika wapo, kuamini kuwa Allah muumba wa vitu vyote yupo, kufa, na kufufuliwa, na kuadhibiwa au kuneemeshwa kaburini, kuumbwa kwa bustani za starehe huko juu na moto huko chini ya ardhi ya chini. Yote haya ni kwa kuwa na imani na sio roho tu, bali tunaamini kuwa wapo watu wapo hai na hawaamini mambo haya pamoja kuwa na roho zao hapa duniani.
Roho hii hutolewa kutoka kwa mtu na malaika maalumu na hapo anakuwa tayari ameshahudhuria mtu huyo kwenye ulimwengu mwingine (wa kaburini) na baada ya kuzikwa mtu huyo anarejeshewa roho yake kwa ajili ya kuadhibiwa au kuneemeshwa kaburini hapo, na haya ni katika yale ambayo yanaaminika ni mambo ya ghaibu (yasiyoonekana kwa macho) isipokuwa ni kwa kuamini tu kwa moyo.
Na moyo ndio ambao unamfanya mtu awe ni mzuri wa tabia au awe ni mbaya kitabia, na pindi kinapotengamaa hiki kipande cha nyama (moyo) basi na vitendo vyake vinakuwa vizuri.
![]() |
Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu mada hii kama historia yake au uenezi wake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |